Timu ya Manchester City ni
wameibuka mabingwa wa kombe la Capital One baada ya kuwabwaga Sunderland
magoli 3-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa uwanja wa Wembley,
Jumapili.
Sunderland ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na mshambuliaji wake Fabio Borini katika dakika ya kumi ya mchezo.Kipindi cha pili Manchester City ilidhamiria kupata ushindi huku wakizidisha mashambulizi langoni mwa Sunderland.
Juhudi zao zilianza kuzaa matunda, ambapo katika dakika ya 55 Yaya Toure alifyatua kombora lililotinga wavuni moja kwa moja na kuisawazishia timu yake. Dakika moja baadaye dakika ya 56, Samir Nasri alifunga bao la pili kwa mkwaju mkali na kumwaacha mlinda mlango wa Sunderland, Mannone akishangaa kinachotokea.
Jesus Navas ambaye alichukua nafasi ya Kun Aguero, alikomelea msumari wa moto katika jeneza la Sunderland baada ya kupachika goli la tatu katika dakika ya 90.
Hadi mwisho wa mchezo vijana wa Pellegrini waliibuka mashujaa na kutawazwa ubingwa wa kombe hilo la Capital One, likiwa kombe lake la kwanza la ubingwa msimu huu.
0 comments:
Post a Comment