Dar es Salaam. Serikali imetoa
mwelekeo wa Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/15 kuwa ni Sh19.6 trilioni,
ikilinganishwa na Sh18.2 za Bajeti iliyopita.
Vipaumbele vya Bajeti hiyo ni kuendeleza Mpango wa
Maendeleo wa Miaka Mitano ulioanza mwaka 2011 na Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN) ambao unajumuisha maeneo sita ya kitaifa ya kilimo,
elimu, maji, utafutaji wa rasilimali fedha, nishati, uchukuzi na
uboreshaji wa mazingira ya kufanyia biashara.
Katika kuhakikisha inakusanya fedha za kutosha,
Serikali imeahidi kuunda kikosi kazi cha kufuatilia mapato yote
yanayotoka halmashauri zote nchini ili kuondoa visingizio
vilivyojitokeza wakati wa ufuatiliaji wa mapato.
Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Fedha, Saada
Mkuya wakati akiwasilisha mapendekezo ya Bajeti hiyo kwa kamati zote za
Bunge, Dar es Salaam.
Alisema matumizi ya kawaida kwa mwaka ujao wa
fedha yanalenga kufanikisha mambo 20 muhimu, yakiwamo Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa mwaka 2014, Uchaguzi Mkuu 2015, kukamilisha mchakato
wa Katiba na nyongeza ya mishahara na kulipa kwa wakati.
Mkuya alisema makadirio ya matumizi ya maendeleo ni Sh7.7 trilioni sawa na asilimia 39 ya matumizi yote ya Serikali.
Kati ya fedha hizo, miradi ya maendeleo imetengewa
Sh5.4 trilioni sawa na asilimia 27 na matumizi mengine ya maendeleo ni
Sh2.2 trilioni.
Utegemezi
Mkuya alisema katika mwaka unaomalizika, Serikali
ilipanga kukopa Dola 700 milioni za Marekani sawa na Sh1.1 trilioni na
kati ya kiwango hicho, iliambulia mkopo wa Dola 259 milioni hivyo kuweka
nakisi ya Dola441.
Alisema katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali
imekusudia kukopa Sh4.2 trilioni kutoka vyanzo vya mapato vya ndani na
nje ili kuziba pengo la mapato.
Misaada na pato la taifa
Katika mwaka wa 2013/2014, Serikali ilipokea
misaada ya Sh1.1 trilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo ikiwa ni
asilimia 50 ya ahadi ya Sh2.3 trilioni, hivyo kuweka nakisi ya Bajeti ya
Sh1.2 trilioni.
Akiwasilisha Rasimu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka
2014/2015, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen
Wassira alisema deni la Taifa limefikia Sh27.04 trilioni kutoka Sh24
trilioni na kufafanua kuwa ongezeko la deni hilo limetokana na mikopo
mipya ya kibiashara na ya masharti nafuu.
Ukusanyaji mbovu wa mapato
Akizungumzia ukusanyaji wa kodi, Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda alisema kumekuwa na matatizo katika ukusanyaji wa mapato
ya ndani, hasa yasiyotokana na kodi.
“Tumepata changamoto na tunajiuliza kwa nini
hatufikii malengo, lakini tunaamini kwamba tukijipanga vyema kwenye
halmashauri zetu kwa kuzibana vyema, tutaweza kupiga hatua nyingine
kutoka hapa tulipo,” alisema.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment