Kesi inayomkabili kiongozi wa Taasisi ya Kiislamu nchini, Sheikh
Ponda Issa Ponda imeendelea kupigwa kalenda katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro.
Ilielezwa mahakamani hapo jana kuwa kesi hiyo haiwezi kusikilizwa kwa
sasa kwa kuwa jalada lake bado halijarudi kutoka Mahakama Kuu, Kanda ya
Dar es Salaam.
Sheikh Ponda anakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kutotii amri
halali ya iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu, kutoa maneno yenye kuharibu
imani za dini na kushawishi watu kutenda kosa, makosa ambayo anadaiwa
kuyatenda Agosti 10 mwaka jana katika eneo la Uwanja wa Ndege Manispaa
ya Morogoro.
Baada ya kutajwa kwa kesi hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mary Moyo
alisema kesi hiyo itaendelea kutajwa mpaka jalada hilo lililoitishwa
Mahakama Kuu Oktoba 15 litakaporudishwa Mahakama ya Morogoro.
Sheikh Ponda alifikishwa mahakamani hapo jana chini ya ulinzi mkali
wa polisi waliokuwa na sihala za moto, mabomu ya machozi na mbwa huku
wafuasi wake wakizuiwa nje ya uzito wa mahakama hiyo.
Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Lilian Lutabula aliyeshirikiana na mwendesha mashtaka wa polisi, Zabron Msusi wakati upande wa utetezi uliwakilishwa na wakili Josephine Jackson kwa niaba ya wakili Bathoromeo Tarimu anayemtetea Sheikh Ponda.
Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, mshtakiwa Ponda alirudishwa
rumande ambako ataendelea kupafanya kuwa maskani yake hadi Mei 5 mwaka
huu kesi hiyo itakapoendelea kutajwa mahakamani hapo.
0 comments:
Post a Comment