Kamanda Mkuu wa Brigedi ya Izzuddin Qassam tawi la kijeshi la
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina Hamas amesema kuwa, ni
muhali kupatikana makubaliano ya usitishaji vita, bila ya kukomeshwa
mashambulio ya majeshi ya utawala wa Israel na kuondolewa mzingiro wa
Ukanda wa Gaza. Kamanda Muhammad Dhwayf amesisitiza kuwa, usitishaji
vita hautakuwa na maana kama hayatakomeshwa mashambulizi ya kijeshi ya
Israel huko Ghaza na kuondoshwa kikamilifu mzingiro unaowakabili
wananchi wa Palestina katika eneo hilo kwa miaka saba sasa. Wakati
huohuo, Msemaji wa Jeshi la Israel amesema kuwa, jeshi la utawala huo
limewaita askari wengine elfu kumi na sita wa kikosi cha dhiba kwa ajili
ya kushiriki kwenye operesheni za Gaza. Msemaji wa Jeshi la Israel
ameongeza kuwa, kuongezwa wanajeshi hao wa dhiba, kutaifanya idadi ya
askari wa Israel walioko katika mpaka wa Gaza kufikia elfu themanini na
sita. Hayo yanajiri katika hali ambayo, Kanali ya 2 ya Televisheni ya
Israel imetangaza kuwa, zaidi ya askari 140 wa Israel wanapatiwa
matibabu hospitalini, ambapo 16 kati yao wako mahututi. Utawala wa
Israel umekuwa ukificha kutangaza idadi ya wanajeshi wanaouawa au
kujeruhiwa, kwa shabaha ya kukwepa kuwavunja moto wanajeshi wa utawala
huo. Kwa upande mwingine, jeshi la Israel limefanya mashambulizi zaidi
ya elfu arobaini ya ardhini, angani, na baharini dhidi ya Gaza tokea
ulipoanzisha vita dhidi ya eneo hilo yapata zaidi ya wiki tatu
zilizopita. Taarifa zinasema kuwa, jeshi la Israel limeharibu zaidi ya
misikiti 70, huko Ghaza. Inafaa kuashiria hapa kuwa, mmoja katiya
maafisa waandamizi wa jeshi la Marekani amesema kuwa, wiki iliyopita
Washington ililikabidhi jeshi la Israel ghala zake za silaha za
makombora, magari ya kijeshi, zana na mizinga kwa ajili ya kuendesha
operesheni za kijeshi huko Gaza.
0 comments:
Post a Comment