RAIS Jakaya Kikwete amesababisha mageuzi makubwa kwa namna Jamhuri ya Watu wa China inavyowapokea viongozi wageni
kutoka nje ya nchi hiyo kwa kuwa kiongozi wa kwanza duniani kupokewa rasmi na pikipiki za polisi na kuongozwa na pikipiki hizo kwa muda wote wa ziara katika kipindi
cha miaka 10 iliyopita. Rais Kikwete aliyewasili China Oktoba 21,
mwaka huu kwa ziara rasmi ya siku sita kabla ya jana kwenda Vietnam, amekuwa kiongozi wa kwanza wa nje kupokelewa na msafara wa pikipiki tangu Januari Mosi, mwaka 2004, miaka 10 iliyopita wakati China
ilipofuta utaratibu wa misafara ya viongozi kusindikizwa na pikipiki za polisi. Rais Kikwete na msafara wake alipokewa na msafara wa pikipiki wa polisi mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Beijing hadi kwenye Nyumba ya Kufikia Wageni wa
Serikali ya Diaoyutai, katikati ya Jiji la
Beijing na utaratibu huo kuendelea kuongoza msafara wake kwa siku zote alipokuwa China.
Taarifa ya habari iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya China na kukaririwa na Shirika la Habari la nchi hiyo la Xinhua haikutoa sababu zozote za mabadiliko ya sera hiyo. Katika nchi karibu zote duniani, utaratibu wa
viongozi wa nchi mbalimbali kupokelewa kwa misafara ya pikipiki ni protokali ya juu kabisa ambayo pia huongeza usalama wa kiongozi na ni utaratibu wa kawaida katika nchi
nyingi duniani. Tangu kuasisiwa kwake mwaka 1949, Jamhuri ya Watu wa China ilikuwa na utaratibu wa pikipiki za polisi kuongoza misafara ya viongozi, lakini utaratibu huo
ulisimamishwa Januari Mosi, mwaka 2004, kwa sababu ambazo hazijapata kuelezwa. Baada ya kuweka historia hiyo ya kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya kigeni kupokelewa na msafara wake kuongozwa na msururu wa pikipiki nane, jana alianza ziarabyake Vietnam kwa mwaliko wa Truong Tan Sang, Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam ambako miongoni mwa mambo mengine nchi hizo mbili zitaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa
kibalozi kati ya nchi hizo mbili.
Miongoni mwa shughuli zake kubwa, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam, Nguyen Phu Trong na Mwenyekiti wa Bunge la Vietnam, Nguyen
Sinh Hung. Aidha, Rais atatembelea taasisi mbalimbali zenye uhusiano wa kiuchumi na Tanzania ikiwemo Kampuni ya Viettel inayotaka kuwekeza katika mawasiliano ya simu za maeneo ya vijijini katika Tanzania kwa bei nafuu zaidi.
0 comments:
Post a Comment