pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Kampuni 35,000 hatarini kufutwa


ZAIDI ya kampuni 35,000 ziko hatarini kufutiwa leseni na wahusika kufikishwa mahakamani kwa kutofuata sheria za uendeshaji biashara nchini.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA), Frank Kanyusi, amesema jana mjini Mwanza baada ya miezi mitatu kuanzia sasa kampuni hizo zitaanza kufutwa.
"Tunatoa miezi mitatu kuanzia sasa kwa wamiliki wa kampuni kuhakikisha wanakamilisha taratibu za uendeshaji wa kampuni zao," amesema.
Ametoa mwito kwa wanaoziendesha kuwasilisha taarifa za kampuni zao kila mwaka pamoja na nakala ya mkaguzi wa fedha, na kwamba kutofanya hivyo kusababisha kufungwa kwa kampuni na kufikishwa mahakamani kwa kukiuka sheria.
"Zaidi ya kampuni 35, 000 zitafutwa na kufunguliwa kesi kwa kutotii sheria na kanuni za uwasilishaji wa taarifa za kampuni kila mwaka," Kanyusi aliwaeleza waandishi wa habari wakati wa usajili wa majina ya biashara na kampuni mkoani hapa.
Amewataka wafanyabiashara na wajasiriamali nchini kutumia fursa ya uwepo wake kurasimisha biashara zao ili serikali iwatambue na kutoa ushirikiano katika kufanya biashara.
Kwa mujibu wake, mwitikio wa watu katika zoezi hilo ni mkubwa kwani wameweza kusajili majina ya biashara 150 na kampuni 100 kwa siku sita kutokana na semina elekezi iliyotolewa kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara.
Alisema wakala unatambua changamoto iliyopo ya upatikanaji wa elimu ya huduma wanazotoa na ndio sababu wameanza ziara ya kutembea mikoa kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi juu ya huduma za Brela na umuhimu wa kurasimisha biashara.
Alifafanua kwa sasa vyombo vya fedha vinaweza kupata taarifa za uhalali wa biashara ya mteja anayetaka kufungua akaunti kupitia mtandao wa Brela.
"Hii itasaidia kuboresha mazingira ya biashara nchini kwani itampa nafuu mteja muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo," alisema Kanyusi.
Alisisitiza kuwa Brela itazindua mfumo wa usajili wa kampuni Machi mwakani ambao utahusisha taasisi nyingine za serikali kama Mamlaka ya Mapato (TRA) ili kurahisisha urasimishaji wa kampuni, ikiwa ni jitihada za kuweka mazingira bora ya biashara nchini.
Alifafanua kuwa mteja atakapowasilisha maombi ya kufungua kampuni, mfumo utamuunganisha na TRA kupata namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN) kwa muda mfupi na mteja atakuwa amekamilisha taratibu na kuendelea na biashara.
Mmoja wa wajasiriamali aliyejitokeza, Gerald Malamba aliwataka wajasiriamali wenzake kurasimisha biashara zao ili kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara na pia serikali kuweza kutambua walipa kodi wake.
Mjasiriamali, Anitha Samson alisema ni faraja kwake kwa Brela kufika Mwanza kwani wamepata elimu juu ya umuhimu wa kurasimisha biashara na kutoa mwito kwa wakala kufungua ofisi za kanda ili kutoa huduma kwa ufanishi zaidi.

0 comments:

Post a Comment