pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Kesi ya Lwakatare yaahirishwa tena


Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Willfred Lwakatare, akipelekwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, chini ya ulinzi wa askari Magereza.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imeiahirisha kesi inayomkabili Mkuu wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na Joseph Ludovick hadi Aprili 17, mwaka huu.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka aliiambia mahakama hiyo iliyokuwa imeketi chini ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana kuwa kesi hiyo jana ilifikishwa kwa ajili ya kutajwa.

Alisema hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba jalada kuu la kesi lipo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Katemana aliiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 17, mwaka huu.
Lwakatare na Ludovick wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama ya kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru Dennis Msacky, kushiriki katika kupanga njama za utekaji nyara, kushiriki katika mkutano wa kupanga kitendo cha ugaidi cha utekaji nyara.

Akisoma hati ya mashtaka hayo, Wakili wa Serikali, Prudence Rweyongeza alidai kuwa washtakiwa walifanya hivyo Desemba 28, mwaka jana katika eneo la King’ong’o wilayani Kinondoni. Washtakiwa kwa pamoja walikula njama kwa kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru Msacky ambaye ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi.

Wakili huyo wa Serikali pia alidai kuwa Desemba 28, 2012 walishirikiana kupanga njama za utekaji nyara dhidi ya Msacky.

mwananchi

0 comments:

Post a Comment