SHIRIKA LA UMEME ZANZIBAR
Tarehe 15/02/2014
TAARIFA KWA UMMA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI JUU YA HALI YA KUKATIKA UMEME ZANZIBAR
Tangu kuanzia mwishoni mwa mwezi Januari, 2014, Zanzibar imeshuhudia
mabadiliko ya hali ya hewa. Mabadiliko ambayo yamekuwa yakiathiri sana
miundo mbinu ya umeme katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Hali ya upatikanaji umeme Zanzibar kwa sasa tokea kuanza kwa mwezi
huu wa pili imekuwa siyo ya kuridhisha katika baadhi ya maeneo.
Umekuwepo ukatikaji wa umeme mara kwa mara hususan katika njia
zinazosafirisha umeme kuelekea mashamba kama vile njia ya Kaskazini,
Kusini, Fumba na baadhi ya maeneo ya mjini.
Kuanguka kwa nguzo za umeme, kupasuka kwa vikombe (pin insulators)
katika njia za kusafirisha umeme pamoja na uchakavu wa miundo mbinu
vimekuwa ni sababu kubwa inayopelekea kukatika kwa umeme mara kwa mara
hivi sasa.
Mvua zinazoendelea kunyesha na upepo unaovuma kwa kasi hupelekea
kuanguka kwa nguzo na hatimae umeme kukosekana. Vilevile, radi
zinazopiga huathiri kwa kuunguza vifaa vilivyo katika miundo mbinu ya
umeme na hatimae pia umeme hukosekana.
Hali hii vile vile inapotokea kwa upande wa Tanzania Bara,
husababisha ongezeko la kasi ya umeme (over voltage) katika njia
inayosafirisha umeme kuleta Zanzibar na hupelekea kisiwa chote kukosa
umeme kama ilivyotokea kwa siku ya Ijumaa ya tarehe 14/02/2014 asubuhi
na usiku.
Katika kushughulikia usalama wa miundo mbinu ya umeme, kama vile
ubadilishaji wa nguzo mbovu, kila siku za Alhamisi na Jumamosi, Shirika
la Umeme (ZECO) linafanya juhudi za kubadilisha nguzo hizo ili kumaliza
kasoro hiyo katika njia zake za kusafirishia umeme. Vilevile, juhudi za
Shirika zimeelekezwa katika kuzifanyia matengenezo ya mara kwa mara njia
zake za ndani zinazosafirisha umeme ili kuondokana na kero za
kukosekana kwa umeme.
Mwisho, Shirika linaomba radhi kwa wananchi na wateja wake ambao
wamekuwa wakipata usumbufu kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme mara
kwa mara.
Aidha, Shirika linahitaji ushirikiano kutoka kwa wateja na wananchi
kwa ujumla kwa kulipatia taarifa Shirika endapo hali yoyote isiyo
salama katika miundo mbinu ya umeme itajitokeza. Taarifa hizo zitatoa
fursa kwa Shirika kuweza kuchukuwa hatua za kuepesha madhara au kero
zinazoweza kutokea. Vile vile Shirika linatoa wito kwa watu wote kuacha
kusogelea au kugusa nyaya za umeme zilizoanguka chini kwani ni hatari
mno.
Kwa kutoa taarifa, tafadhali piga simu nambari 0242 230 232
0 comments:
Post a Comment