Newala. Kutokana na kumwamini mumewe, Rehema
Saidi, mkazi wa kijiji cha Rahaleo, Kata ya Mkunya Wilaya ya Newala
mkoani Mtwara, hakuwahi kutia shaka pale alipomwacha na watoto, wakati
yeye alipolazimika kutoka kwenda sehemu yoyote kwa ajili ya shughuli za
kifamilia.
Rehema na mumewe Juma Malolo waliishi na watoto
wawili; mwenye umri wa mwaka ambaye walimzaa pamoja na mwenye umri wa
miaka tisa ambaye (Rehema) alimzaa kwa mwanamume mwingine kabla ya
kuolewa mara ya pili.
Mwanamama huyu anasema aliishi kwa raha mustarehe
na familia yake na katika mazingira ya kawaida, hakuwahi kuwaza kutokea
kwa kitendo alichokishuhudia Agosti, 14 mwaka jana, pale alipomkuta
mumewe (Malolo) akimbaka binti yake (jina tunalihifadhi).
Rehema anasimulia kwamba siku ya tukio alikuwa
akitoka sokoni alikokwenda kuchuuza mbogamboga kwa ajili ya kupata fedha
za kujikimu yeye na familia yake.
“Niliporudi nyumbani nilifungua mlango bila hata
ya kubisha hodi kwa sababu ni nyumbani kwangu na wala sikuwa na hofu ya
jambo lolote…sikuamini pale nilipomkuta mume wangu akiwa anambaka mtoto
wangu, kwanza nilipigwa na butwaa, nikapandwa na hasira, nilimvamia na
kuanza kumpiga Niliumia sana kiasi siwezi hata kuhadithia aina ya
maumivu niliyoyapata,” anasimulia kwa huzuni.
Anabainisha kuwa baada ya hapo, alitoka nyumbani
hapo kuwaita majirani ili waweze kushuhudia kitendo hicho, lakini
aliporejea hakumkuta mumewe kwani alikuwa ameondoka na kibaya zaidi
alichukua fedha zilizotokana na biashara yake Sh40,000 ambazo zilikuwa
ndiyo akiba pekee aliyokuwa amebaki nayo.
“Nilikwenda kwa baba wa mtoto kumwambia ili
anisadie fedha ya kwenda mjini kutoa taarifa polisi lakini alisema hana
fedha. Hivyo nilishindwa kwenda na hata hospitali kumpima, kwa sababu
sikuwa na fedha tena ...nilibaki nyumbani huku nikilalamika kwa kitendo
alichofanyiwa mwanangu,” anasema Mariam.
Anaeleza kuwa alikaa siku tatu bila kumwogesha
binti yake kwa lengo la kutunza ushahidi wa kitendo alichofanyiwa na
wakati huo alikuwa akitafuta fedha ili aende polisi na baadaye kumpeleka
hospitali, lakini hakufanikiwa.
Mariam anasema baada ya siku tatu kupita huku
akiwa amepoteza matumaini ya kupata nauli, alimwogesha mtoto huyo, hivyo
ni dhahiri kwamba alipoteza ushahidi wa kitendo alichofanyiwa.
Ilikuwaje?
Rehema anasema siku ya tukio, Agosti 14 mwaka jana
aliondoka nyumbani kwake saa 11 alfajiri kwenda shambani kwa Mzee
Makwedu umbali wa kilomita tatu kutoka kijijini kwake, kununua majani ya
kunde ili ayapeleke Mjini Newala kuyauza.
Anasema alimwacha mumewe na watoto wawili.
“Nilimuaga mume wangu na kumwacha na watoto wote wawili, kwa kuwa
nilimwacha na mtoto mchanga wa mwaka mmoja niliamua kufanya haraka ili
asije akaanza kulia wakati sijarudi,” anasimulia na kuongeza:
“Kwa hiyo nilikuwa nakimbia wakati wa kwenda na hata wakati wa kurudi, lakini nilichokiambulia ni hicho nilichokiona.”
Anasema katika miaka miwili ya ndoa aliyoishi na
Malolo hakuwahi kuwa na shaka juu ya binti yake, kwani alihakikisha
anamtimizia mumewe mahitaji yote ya ndoa.
“Kama mwanadamu niliwahi kuwaza kwamba mume wangu
angeweza akawa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine, lakini
sikuwahi kufikiri kuwa anaweza kumgeuza binti yake kuwa ‘mke mwenza
wangu’,” anasema Mariam.
Kwa upande wake binti aliyebakwa mwenye umri wa
miaka tisa (jina tunalihifadhi), anakiri kwamba baba yake huyo wa
kufikia amekuwa akimfanyia vitendo hivyo mara kwa mara, huku akimtisha
kumchinja iwapo angetoa taarifa kwa mama yake au mtu mwingine yeyote.
“Alikuwa akinifanyia mara kwa mara, mama
anapoondoka kwenda katika shughuli zake za biashara ya mboga, alikuwa
ananiita na kuniambia njoo ndani tufanye mambo na kunikataza nisiseme
nikisema atanichija,” anasimulia binti huyo.
Hija Ahmad ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha
Rahaleo, anasema alishtushwa na tukio hilo ingawa juhudi za kumnasa
mwanamume huyo hazijazaa matunda hadi sasa.
Ahmad anasema binti huyo kwa umri alionao,
anahitaji msaada wa matibabu ya kisaikolojia. “Mtoto huyu kwa sasa
ameathirika kisaikolojia kutokana na kuzomewa na wenzake, mara nyingi
utamkuta amejitenga ….nadhani unahitajika msaada wa kumtibu
kisaikolojia,” anasema.
Katibu wa asasi ya kutetea haki za wanawake
wilayani Newala (NEWORA), Mwanahamisi Fakihi anathibitisha kupokea
taarifa za tukio hilo na kwamba jitihada zinaendelea kumsaka muhusika
ili afikishwe mahakamani.
Ubakaji Newala
Mganga Mkuu wa Hospital ya Wilaya ya Newala, Dk.
Yudas Ndungile anasema matukio ya ubakaji yameongezeka katika wilaya yao
na takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2012 walipokea kesi saba za ubakaji na
mwaka jana kesi 11.
“Matukio ya ubakaji ni hatari kwa afya za wabakaji
na wabakwaji, unajua kuna maradhi ya ngono ikiwa pamoja na Ukimwi, pia
watoto wanaobakwa husababishiwa madhara makubwa ya kisaikolojia, wito
wangu kwa jamii iamke kupambana na vitendo hivi vya ubakaji,” anasema
Dk. Ndungile.
Karani wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Newala, Maweda
Samuel anasema mwaka 2012 walipokea kesi saba za ubakaji na kati ya
hizo, kesi namba 134 ilivunja rekodi kwani washtakiwa watatu walitiwa
hatiani kwa kumbaka mwalimu na wote walihukumiwa kwenda jela.
Samuel anasema kuwa mwaka jana kulikuwa na kesi 11 za ubakaji
mojawapo ikiwa ni ileinayomuhusu mshtakiwa anayetuhumiwa kwamba
alimlawiti mbuzi hadi kufa. Mshtakiwa huyo yupo mahabusu hadi sasa
kutokana na jamii kutaa kumwekea dhamana kutokana na kuchukizwa na
kitendo hicho.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Newala, George
Martin anasema vitendo vya ubakaji kwa watoto vinashamiri katika wilaya
hiyo na kuhusisha na imani ya kishirikina kuhu akieleleza kuwa tiba yake
ni kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za vitendo hivyo.
“Kwanza jamii ishirikiane na polisi katika
kuwafichua wahalifu wa matukio haya ili sheria ifanye kazi yake na kutoa
fundisho kwa wengine,” anasema Martin.
Mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Magala anasema
vitendo vya ubakaji havikubaliki ndani ya jamii na kusisitiza kuwa
watakaobainika kujihusisha na tabia hizo watachukuliwa hatua za
kisheria.
“Wananchi wasisubiri mambo yaharibike ili
tulaumiane, wahakikishe wanatoa taarifa hata kama ni za siri polisi au
mahala husika ili wabakaji wadhibitiwe,” anasema Magala.
Vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ukiwamo
ubakaji, vinaendelea kushamiri nchini licha ya kuwepo kwa sheria ya
makosa ya kujamiana ya 1998 (SOSPA) inayotoa adhabu ya kifungo cha
maisha jela au miaka isiyopungua 30 kwa mtu anayepatikana na hatia kwa
kosa hilo.
Tafiti zilizofanywa na Chama cha Waandishi wa
Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) zinathibitisha kwamba vitendo vya
ukatili hususan ubakaji ni vingi katika jamii, chanzo kikuu kikiwa ni
kuporomoka kwa maadili na athari za utandawazi.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment