RAIS
Jakaya Kikwete ametoa tuzo ya Kiongozi Bora wa Maendeleo Afrika
aliyoipata hivi karibuni kwa ajili ya Watanzania wote ili kuonyesha
heshima kwao.
Alisema Watanzania wamechangia katika maendeleo yaliyomwezesha
kutunukiwa tuzo hiyo ya kimataifa, hivyo ni zawadi kwa ajili ya
Watanzania wote popote walipo.
“Napokea tuzo hii kwa niaba ya Watanzania wote… naitoa kwa Watanzania
kwa sababu hata kama nimekuwa kiongozi ukweli ni kwamba mafanikio na
maendeleo yote yaliyopatikana na kuipata tuzo hii yametokana na juhudi
zetu za pamoja,” alisema.
Rais Kikwete alipokea tuzo ya Kiongozi Bora wa Maendeleo Afrika mwaka
2013 kwa kuwa kiongozi wa utumishi bora kwa umma Afrika na aliyetoa
mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya uchumi wa wananchi wake kutoka kwa
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
kwenye halfa iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana asubuhi.
Waziri Membe alipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Kikwete katika
sherehe zilizofanyika kwenye Hoteli ya St. Regis jijini Washington,
Marekani usiku wa Aprili 9, mwaka 2014.
Tuzo hiyo hutolewa kila mwaka na jarida maarufu la kimataifa la
African Leadership Magazine kwa kiongozi wa Afrika aliyetoa mchango
mkubwa zaidi wa maendeleo kiuchumi kwa wananchi wake na Rais Kikwete
alikuwa rais wa tatu Afrika kupokea tuzo hiyo.
Tuzo hiyo iliwahi kutolewa pia kwa marais wa Sierra leone na Liberia kabla ya kupewa Rais Kikwete.
Akipokea tuzo hiyo mbele ya waandishi wa habari, Rais Kikwete alisema
ina maana kuwa dunia inaona, inatambua na inathamini kazi inayofanywa
na Watanzania katika jitihada za kujiletea maendeleo.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa Waziri Membe na Balozi wa Nigeria nchini
Marekani, Profesa Ade Adefuye, kwa niaba ya Rais Goodluck Jonathan
ambaye awali alipangwa kukabidhi tuzo hiyo kwa Rais Kikwete.
Profesa Adefuye alisema: “Kwa niaba ya Nigeria na kwa niaba ya Bara
la Afrika nawasilisha kwenu Mwafrika wa wakati huu, mtoto maarufu wa
Tanzania na mtoto maarufu wa Afrika, Rais Jakaya Kikwete.”
0 comments:
Post a Comment