MBUNGE
wa Rungwe Mashariki na Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu, Profesa Mark
Mwandosya, amefunguka kwa mara ya kwanza na kuelezea mwelekeo wake wa
kisiasa na hasa nia yake ya kuwania urais mwaka 2015.
Mwandosya,
ambaye alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na Mtanzania,
tayari ameeleza wazi kuwa hatatetea tena kiti chake cha ubunge mwaka
2015.
Akizungumzia
suala la urais, Mwandosya, ambaye amewahi kuwania nafasi ya kuteuliwa
na chama kugombea urais mwaka 2005, akichuana na Rais Jakaya Kikwete,
alisema itakuwa heshima kwake kama chama kitaweza kumfikiria na
hatimaye kumteua kugombea urais mwaka 2015.
“Kuteuliwa
na chama kuwa mgombea urais ni heshima kubwa na ni kilele cha utumishi
ambao mwanachama anaweza kutoa kwa chama na kwa Taifa. Itakuwa ni
heshima iliyoje kwangu iwapo chama kitaweza kunifikiria na hatimaye
kuniteua kufika hapo,” alisema Mwandosya katika mahojiano hayo.
Hata
hivyo, Mwandosya alisema tusimtake avuke daraja hata kabla ya kulifikia
asije akatumbukia kwenye maji au kama mto hauna maji basi asianguke
kwenye mawe.
Bila
kufafanua kauli yake hiyo ina maana gani, Mwandosya alikumbusha jinsi
uamuzi wake wa kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais mwaka 2005
ilivyomjengea heshima na kumtia moyo.
“Mtakumbuka
tarehe 4 Mei mwaka 2005 nilikuwa mmoja wa wanachama watatu tuliopewa
heshima kubwa ya kufika Chimwaga mbele ya Mkutano Mkuu wa CCM (Taifa).
“Wengine
walikuwa Jakaya Kikwete na Dk. Salim Ahmed Salim. Katika uchaguzi huo
Kikwete alipata tuzo ya ‘dhahabu’, Dk Salim alipata tuzo ya ‘fedha’ na
mimi nikapata tuzo ya ‘shaba’.
“Niliwashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu na chama kwa ujumla na kusema ‘shaba si haba’. Angalau nina mtaji wa kuanzia,” alisema Mwandosya.
Miaka
miwili iliyopita, Mwandosya ambaye alikuwa akikabiliwa na maradhi,
alikaririwa akisema kuwa hatakuwa tayari kuzungumzia urais na badala
yake alikuwa ameelekeza akili yake katika kuhakikisha afya yake
inaimarika kwanza ndipo azungumzie mustakabali wake wa siasa za 2015.
Kauli
yake hiyo aliitoa mara baada ya Rais Jakaya Kikwete kumuapisha Ikulu,
jijini Dar es Salaam kutokana na kuwepo nchini India kwa matibabu wakati
mawaziri wapya wakiapishwa.
Akizungumzia
hali yake ya kiafya kwa sasa, Mwandosya alisema anamshukuru Mungu kwa
uponyaji, kwani miaka mitatu iliyopita ilikuwa ni yenye changamoto kubwa
kwake.
“Ni
kweli miaka mitatu iliyopita imekuwa yenye changamoto kubwa kwangu
kiafya na hivyo kwa familia yangu na Watanzania wenzangu. Kabla
sijaugua ghafla mwaka 2011, nilikuwa sijawahi kulazwa hospitali.
“Nilikuwa
nikienda hospitali kuwajulia hali wagonjwa. Wahenga wanasema hakika
‘hujafa hujaumbika’. Nimechukulia kuumwa kama vile ni mtihani katika
maisha, kwamba binadamu inapaswa apitie ili awe kamili.
“Bila
shaka unaweza kudhihirisha kwamba ile picha wakati Rais ananisaidia
kushuka ngazi za Ikulu baada ya kuniapisha kuwa Waziri wa Nchi katika
Ofisi yake na mnavyoniona sasa ni tofauti kabisa. Namshukuru Mwenyezi
Mungu, muweza wa vyote kwa uponyaji,” alisema Mwandosya.
Pia alisema kuwa anawashukuru Watanzania wengi ambao walimuweka katika dua, maombi na sala.
“Sina cha kuwalipa isipokuwa kujitahidi, kwa kadri Maulana atakavyonijalia, kutoa utumishi uliotukuka,” alisema Mwandosya.
Kwa
mara ya kwanza, Profesa Mwandosya alipelekwa nchini India kwa matibabu
mwaka 2011 na kurejea nchini Novemba 29, akiwa amekaa nchini humo kwa
miezi mitano.
Mwandosya
ambaye pia ni Mbunge wa Rungwe Mashariki, ni miongoni mwa wanasiasa
ambao wamekuwa wakitajwa kuwania urais mwaka 2015, baada ya kushindwa
kupata nafasi hiyo alipojitosa mwaka 2005.
Baada
ya uchaguzi wa mwaka 2005 na ule wa 2010 uliompa ushindi Rais Jakaya
Kikwete, Profesa Mwandosya, ambaye si mzungumzaji, alipata kuhisiwa na
kundi la wanamtandao akidaiwa kushirikiana na Mbunge wa Kyela, Dk.
Harrison Mwakyembe, anayetoka naye mkoa mmoja.
Pamoja
na Mwakyembe, katika kundi hilo ilidaiwa kuwa wamo pia Waziri wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta pamoja na wanasiasa wengine ambao wakati huo
walionekana kujinasibu na mapambano dhidi ya ufisadi.
Hata
hivyo, baada ya afya ya Mwandosya kuanza kuzorota, matumaini ya
mwanasiasa huyo kuwania urais yakaanza kufifia, fursa ambayo wachambuzi
na wadadisi wa mambo wanadai kuwa imechukuliwa na Sitta, ambaye tayari
ameshatangaza azma yake ya kugombea nafasi hiyo mwaka 2015.
Mei
2013, Waziri Sitta akiwa kwenye Kongamano la Mawasiliano katika Nyanja
za Digitali la wanafunzi wa Idara ya Uhusiano na Masoko, Chuo Kikuu cha
St. Augustine, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa wakati
ukifika, yeye na rafiki zake watachagua mmoja wao watakayeona anafaa
kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Bila
kulitaja jina la Mwandosya, Sitta aliwataja marafiki zake hao kuwa ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe.
Siku
chache baada ya Sitta kumhusisha Dk Magufuli na kundi la urais la mwaka
2015, Waziri huyo aliibuka na kupinga kauli hiyo, akisisitiza hafikirii
kuwania nafasi hiyo.
Mbali
na Mwandosya, ndani ya Chama Cha Mapinduzi wengine wanaotajwa kuwania
nafasi hiyo ni mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward
Lowassa.
Wengine
ni Waziri Membe, Sitta, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba, ambaye tayari amekwisha tangaza msimamo
wake wa kugombea urais mwaka 2015.
Katika
kinyang’anyiro hicho yumo pia aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani,
Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William
Ngeleja, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) Stephen
Wassira, Rais wa Zanzibar, Dk Mohammed Shein.
Hata hivyo katikati ya mbio hizo za urais, imeibuka hoja mpya ya ujana na uzee.
Hoja
hiyo tayari imewagawa Watanzania katika makundi mawili, moja likipigia
chapuo vijana na jingine wazee, kwa madai kuwa nafasi ya urais ni nyeti
hivyo inahitaji mtu aliyekomaa.
Credit: Mtanzania
Credit: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment