MABASI mawili yamegongana uso kwa uso
wilayani Sikonge mkoani Tabora na kuua abiria 13, wakiwemo madereva wa
mabasi hayo na kujeruhi wengine 73. Moja ya mabasi hayo, lilikuwa
likitokea mkoani Mwanza kwenda Mpanda na lingine likitokea mkoani Mbeya
kwenda Mwanza.
Taarifa kutoka eneo la tukio, ilieleza
kuwa mabasi hayo yalipata ajali hiyo jana saa 10.05 jioni katika eneo la
Mlogoro, kilometa tatu kabla ya kuingia katika mji wa Sikonge.
Mabasi hayo moja linamilikiwa na Kampuni
ya AM Investment Namba T 803 ATN, lililokuwa likitokea Mwanza kwenda
Mpanda. Lingine ni mali ya kampuni ya Sabena Namba T 110 ARV, lililokuwa
likitokea Mbeya kwenda jijini Mwanza.
Akizungumza na mwandishi wetu jana
jioni, Kaimu Mganga wa Wilaya ya Sikonge, Dk John Buswelu, alisema
hospitali hiyo ilikuwa imeshapokea miili 13 ya abiria waliokufa, huku
mmoja ukiwa kiwiliwili bila kichwa.
Shuhuda wa ajali hiyo aliyekuwa sehemu
ya tukio, Suleimani Kambuzi alidai majeruhi waliotolewa katika ajali
hiyo, walikuwa zaidi ya 70.
Alidai wengine walikuwa wakiendelea
kutolewa na kupelekwa hospitalini. Mwandishi alimtafuta Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, ambaye alikiri kufahamu kutokea
kwa ajali hiyo.
Aliongeza kuwa taarifa rasmi ataitoa leo.
Ajali hiyo imetokea wakati Watanzania hawajasahau ajali iliyotokea
wakati wa Sikukuu ya Idd el Fitri mwezi uliopita, na kuua watu 17 katika
eneo la Pandambili wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Ajali hiyo ilihusisha basi la kampuni ya
Moro Best, lenye namba za usajili T 258 AHV lililokuwa likitoka Mpwapwa
kwenda Dar es Salaam.
Basi hilo liligongana uso kwa uso na lori
la mizigo, lenye namba za usajili T820 CKU -T 390 CKT, lililokuwa
likitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma.
0 comments:
Post a Comment