Ndege na vifaru vya utawala haramu wa Kizayuni zimeanzisha tena
wimbi la mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Ghaza baada ya kumalizika
muhula wa usitishaji vita wa masaa 72. Maeneo kadhaa ya ukanda huo leo
yameshuhudia mashambulizi ya Wazayuni yaliyopelekea kwa uchache mtoto
mmoja wa miaka 6 kuuawa shahidi na watu kadhaa kujeruhiwa. Utawala wa
Kizayuni umetangaza kuwa, umeanzisha mashambulizi hayo baada ya
kumalizika muda wa masaa 72 na kushindikana kuongezwa muda usitishaji
vita huo. Kwa upande wake muqawama umejibu mashambulizi hayo kwa
kuvilenga vitongoji kadhaa vya walowezi wa Kizayuni na kufanya walowezi
wengi kukumbwa na wahka mkubwa sanjari na kupigwa ving'ora vya hatari
katika miji mingi ya Israel. Hii ni katika hali ambayo Fauz Barhum,
Msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Palestina HAMAS asema kuwa, makundi
ya muqawama ya Palestina, yamepinga kuongezwa muda wa usitishaji vita na
utawala wa Kizayuni, kutokana na Israel kushindwa kutekeleza masharti
yao ikiwemo kuacha kuuzingira ukanda huo. Katika upande mwingine,
viongozi wa Misri leo wameruhusu kufunguliwa kivuko cha Rafah kwa lengo
la kupitisha majeruhi wa Ukanda wa Ghaza kwenda kutibiwa nchini humo.
Viongozi wa serikali ya Cairo wametangaza kuwa, hatua hiyo imechukuliwa
kwa ajili tu ya kuwaruhusu majeruhi na kwamba hadi sasa bado mawasiliano
ya kina yanaendelea kuhusu suala hilo. Vyombo vya habari vimeripoti
kuwa hadi sasa ni majeruhi 500 pekee waliokwishavuka katika kivuko
hicho, tangu yalipoanza mashambulizi ya kinyama ya utawala haramu wa
Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza. Hii ni katika hali ambayo serikali ya
Cairo ilikuwa imekataa kufungua kivuko hicho na hivyo kufanya hali ya
mambo kuwa mbaya zaidi kwa wakazi wa Ukanda wa Ghaza. Aidha Misri
imetangaza kuwa, misaada ya kibinaadamu na tani saba za madawa na zana
za kitiba zimeruhusiwa kuingia huko Ghaza mapema leo Ijumaa






0 comments:
Post a Comment