
Jeshi la utawala haramu wa Israel limewaua watoto zaidi ya 350 hadi sasa katika hujuma yake inayoendelea katika Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, watoto hao wameuawa tokea
Israel ianzishe hujuma yake ya kinyama dhidi ya Ghaza Julai 8. Taarifa
hiyo imeongeza kuwa watoto pia ni thuluthi moja ya zaidi ya Wapalestina
9,000 waliojeruhiwa huko Ghaza.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo utawala haramu wa Israel ungali
unaendeleza hujuma yake za kinyama dhidi ya Ukanda wa Ghaza. Hadi sasa
zaidi ya Wapalestina 1,700 wameuawa shahidi katika hujuma ya kikatili ya
Israel dhidi ya eneo hilo ambalo pia liko chini ya mzingiro. Kwa ujumla
ni kuwa, asilimia 80 ya waliouawa katika hujuma ya Israel huko Ghaza ni
raia wakiwemo wanawake 200 na wafanyakazi wa sekta ya afya.
Wakati huo huo msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya
Palestina Hamas, Sami Abu Zuhri ameituhumu Israel kwa kukiuka mapatano
ya usitishaji vita yaliyofikiwa Ijumaa kwa upatanishi wa Umoja wa
Mataifa. Amesema Israel ilijaribu kutumia mapatano hayo kujipenyeza
zaidi Ghaza na kwamba wanaharakati wa Palestina walikabiliana na hujuma
hiyo kwa lengo la kujihami. Msemaji huyo wa Hamas amesema hatua ya
Israel ya kuwashambulia raia na hasa wanawake na watoto ni ishara kuwa
utawala huo wa Kizayuni umeshindwa vitani.
MISKITI NA MAHOSPITALI

Utawala wa Kizayuni wa Israel haujatosheka kwa kuwaua
kwa umati wanawake na watoto wa Ghaza bali pia umeharibu kwa mabomu
idadi kubwa ya misikiti na mahospitali katika ardhi hiyo ya Wapalestina.
Kanali ya Televisheni ya Al Mayadeen imeripoti kuwa katika
hujuma ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza
mahospitali na vituo vya afya 44 vimeharibiwa kabisa. Hivi sasa aghalabu
ya Wapalestina waliojeruihiwa katika vita vya Ghaza hawana sehemu za
kupata matibabu. Mbali na kubomoa mahospitali, jeshi la Kizayuni pia
limeharibu kabisa misikiti 41 katika Ukanda wa Ghaza. Kwa mujibu wa
ripoti hiyo, jeshi la utawala haramu wa Israel limeshambulia na kubomoa
misikiti hiyo ambayo ilikuwa sehemu ya hifadhi ya Wapalestina ambao
nyumba zao zimeharibiwa kwa mabomu.
Wakati huo huo katika kujibu jinai za utawala wa Kizayuni
wa Israel, Brigedi ya Izzuddin Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya
Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imevurumisha makombora katika
miji inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Aidha wanamapambano ya
Palestina wamefanikiwa kuwaangamiza wanajeshi wasipungua 131 wa utawala
wa Kizayuni katika vita vya Ghaza.
0 comments:
Post a Comment