Fahad Musana, ambaye ni shabiki wa kutupwa wa klabu ya soka ya
Chelsea, amefariki dunia baada ya mchezaji wa zamani wa klabu hiyo,
Frank lampard, kuifungia Manchester City bao la kusawazisha, katika
pambano lililopigwa jana baina ya timu hizo mbili.
Musana, mwenye umri wa miaka 24, na ambaye alikuwa mcheza kandanda
la kulipwa nchini Uganda, alikuwa akitizama mechi hiyo iliyovuta hisia
za mashabiki wengi katika kona mbalimbali za dunia, na alianguka na
kuzimia mara baada ya Lampard kusawazisha bao, ikiwa ni dakika chache
sana tangu aingie kutokea benchi, katika dakika za lala salama.
Alithibitishwa kuwa amefariki baada ya kuwasili katika hospitali ya
kijeshi ya Bombo, na rafiki wa karibu wa marehemu amenukuliwa na vyombo
vya habari akisema “Jamaa, amekuwa ni shabiki wa kweli wa Chelsea,
ambaye angeweza kufanya lolote lile kwa ajili ya klabu hiyo. Tulifanya
naye mazoezi asubuhi ya jumapili, na hata mchana tukala chakula cha
mchana pamoja, hakika inasikitisha”
Tukio hili la kusikitisha, limethibitishwa na Shirikisho la vyama
vya soka nchini Uganda (FUFA), ambalo limetoa tamko lake kufuatia mkasa
huu wa kushtusha.
“FUFA, limekumbwa na mshtuko baada ya kupokea taarifa za kifo cha
ghafla cha mchezaji wa klabu ya Simba ya Uganda, Misana Fahad, katika
hospitali ya Bombo. Mwili wa marehemu bado uko hospitalini hapo, na
taratibu za mazishi zinaandaliwa na taarifa zitatolewa baadae”, sehemu
ya taarifa ya FUFA imesomeka hivyo.
Hii si mara ya kwanza kwa mashabiki wa soka kufariki kufuatia timu
wanazozishabikia kushindwa kuibuka na ushindi katika mechi zao.
Kumbukumbu za hivi karibuni sana kwa ukanda wetu wa Afrika Mashariki na
Kati, ni za shabiki mwingine wa soka aliyefariki dunia msimu uliopita,
baada ya timu aliyokuwa akiishabikia ya Manchester United kupoteza moja
ya mapambano yake, ilipokuwa chini ya kocha David Moyes
0 comments:
Post a Comment