Baada ya kutangazwa kifo
cha Mfalme Abdullah bin Abdulaziz wa Saudi Arabia Ijumaa ya jana, nchi
hiyo sasa imeingia katika mabadiliko ya muundo wa utawala na madaraka.
Mwili wa Mfalme Abdullah aliyekuwa na umri wa miaka 91 ulizikwa jana
Ijumaa katika mazishi yaliyohudhuriwa na wanawafalme kadhaa na kwa
utaratibu huo uongozi wa Salman bin Abdulaziz ulianza rasmi.
Katika ujumbe wake wa kwanza
kwa mnasaba wa kushika madaraka ya nchi, Mfalme mpya wa Saudia alisema
kwamba, atadumisha sera za wafalme wa kabla yake. Ujumbe huo una maana
kwamba, hatafanya mabadiliko katika siasa za ufalme wa nchi hiyo. Suala
hilo lilikuwa likitarajiwa na wengi kwa kutulia maanani sera za utawala
wa kifalme wa Saudi Arabia. Hata hivyo suala lililoelekeza macho ya
wachambuzi wa mambo kwenye mabadiliko ya utawala huko Saudia baada ya
kufariki dunia Mfalme Abdullah Ijumaa ya jana ni hatua ya mfalme mpya ya
kuuzulu na kuteua baadhi ya watu kushika nafasi muhimu katika serikali
ya nchi hiyo. Jambo hilo limewashangaza wengi hasa kwa kutilia maanani
kwamba, amri za kuteua na kuuzulu baadhi ya maafisa wa ngazi za juu wa
serikali ilitolewa hata kabla ya kuzikwa mwili wa Mfalme Abdullah.
Mfalme Salman alimteua Muqrin bin Abdulaziz kuwa Mrithi wa Kiti cha
Ufalme. Muqrin anatajwa kuwa ni mtu anayeweza kushika hatamu za ufalme
wa Saudia mapema na haraka. Hii ni kwa sababu Salman bin Abdulaziz sasa
ameingia katika mwaka wa 80.
Mfalme mpya wa Saudia pia
alimteua Muhammad bin Nayif kuwa Mrithi wa Mrithi wa Kiti cha Ufalme na
Naibu wa Pili wa Waziri Mkuu wa Saudia. Vilevile alimteua mwanawe,
Muhammad bin Salman, kuwa Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia na Mkuu wa
Idara ya Mfalme wa nchi hiyo. Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mafuta
wamebakishwa katika nafasi zao.
Nukta ya kutiliwa maana hapa
ni kwamba, upinzani wa kwanza dhidi ya hatua ya Mfalme Salman baada tu
ya kuteuliwa na kuondolewa madarakani baadhi ya maafisa wa utawala wa
kifalme wa Saudia, umetokea ndani ya utawala huo. Mut’ab bin Abdullah,
mwana wa mfalme aliyefariki dunia ambaye ni Waziri wa Gadi ya Taifa ya
Saudi Arabia amekasirishwa sana na hatua hiyo na kusema kuwa amekuwa
mhanga wa mchezo wa kisiasa wa mfalme mpya wa nchi hiyo. Mut’ab anaamini
kuwa Mfalme Salman amekhitari siasa za kuwaengua watu wote waliokuwa
karibu na baba yake. Mtazamo huo unapata nguvu zaidi kwa kuzingatia kuwa
Mut’ab bin Abdulllah hakupewa nafasi yoyote nyingine lakini mpinzani
wake mkubwa yaani Muhammad bin Nayif ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mambo
ya Ndani, ameteuliwa pia kuwa kuwa mrithi wa mrithi wa kiti cha ufalme.
Vilevile kuteuliwa kwa Muhamamd bin Salman kuwa Mkuu wa Idara ya Ufalme
wa Saudia kunamfanya mwana huyo wa mfalme mpya kuwa miongoni mwa
wanamfalme wenye taathira kubwa wa kizazi cha tatu cha utawala wa
Kifalme wa Saudia. Kwa utaratibu huo wachambuzi wa mambo wanasema, hatua
hiyo ya Mfalme Salman imetoa pigo kubwa kwa mwana wa mfalme aliyefariki
dunia, Mut’ab bin Abdullah, ambaye alikuwa na matarajio kuwa na nafasi
kubwa katika mustakbali wa utawala wa kizazi hicho.
Ukweli ni kuwa mirengo miwili
ya Sudairi na Shammary imekuwa na mivutano kwa miaka mingi ndani ya
kizazi cha utawala wa kifalme cha Aali Saud kwa ajili ya kudhibiti
utawala na madaraka. Mfalme aliyefariki dunia ni kutoka mrengo wa
Shammari na Salman anatoka mrengo wa upinzani wa Sudairi ambao ndio
wenye nguvu kubwa.
Inaonekana kuwa kushika
madaraka mrengo wa Sudairi kumechochea zaidi vita vya kuwania madaraka
kati ya wanamfalme wa kizazi kipya wa mirengo hiyo miwili hasimu ndani
ya kizazi cha Aal Saud. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, Salman bin
Abdulaziz ambaye inasemekana anasumbulwia na maradhi ya Alzheimer,
hawezi kubakia madarakani kwa kipindi kirefu.
Hapana shaka kuwa kizazi cha
kale cha watawala wa Saudi kinaelekea ukingoni lakini siasa za ndani za
Riyadh bado ni zilezile zilizopitwa na wakati zinazorejea katika kipindi
cha utawala wa Abdulaziz, baba wa wafalme wa Saudia. Ama kuhusu suiasa
za nje za nchi hiyo, kumetokea baadhi ya mabadiliko tangu zama za
Abdulaziz. Kwani kipindi fulani watawala wa kizazi cha Aal Saud walikuwa
tegemezi kwa Uingereza lakini katika miongo ya hivi karibuni watawala
wa kizazi hicho wamekuwa watekelezaji kamili wa sera za Washington.
Baada tu ya kushika madaraka, Mfalme Salman ametilia mkazo kwamba
atadumisha njia ya waliomtangulia, suala ambalo lina maana ya kudumisha
ushirikiano wa Saudia na Magharibi hususan Marekani katika nyanja zote
ikiwa ni pamoja na katika sera za mafuta, ugaidi na hata jinsi ya
kuamiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel.
0 comments:
Post a Comment