Dar es Salaam. Hali bado ni tete kwa mawaziri wakati Rais Jakaya Kikwete akiwasiliana na viongozi waandamizi kabla ya kutangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri baada ya kuwa na vikao kadhaa jana na vigogo katika kile kinachoonekana kupata ushauri.
Rais anatarajiwa kutangaza mabadiliko makubwa au
madogo wakati wowote, ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano
kuhusu sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya
Tegeta Escrow kabla ya chombo hicho cha kutunga sheria kuanza vikao
vyake Jumanne ijayo mjini Dodoma.
Sakata hilo, lililohusu takriban Sh306 bilioni
zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lilisababisha Anna Tibaijuka
kuvuliwa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na
kubainika kuingiziwa Sh1.6 bilioni na mmiliki wa zamani wa Kampuni ya
IPTL iliyo na mkataba na Shirika la Umeme (Tanesco) wa kuizuia nishati
hiyo.
Profesa Sospeter Muhongo, ambaye ni Waziri wa
Nishati na Madini anatakiwa aondolewe kwa mujibu wa maazimio ya Bunge na
hivyo kuwapo kwa nafasi mbili ambazo Rais atalazimika kuziziba kwa
kufanya mabadiliko madogo au makubwa kwenye baraza hilo.
Kwa mujibu wa habari ambazo gazeti hili ilizipata
jana kutoka vyanzo mbalimbali, vigogo kadhaa wa Serikali waliitwa Ikulu
kwa ajili vikao ambavyo inaaminika kuwa vya kujadili jinsi ya kumaliza
sakata hilo, ambalo linafuatiliwa na wananchi na nchi wahisani.
Hata hivyo, wapashaji wetu hawakuweka bayana kuwa
vikao hivyo vinahusu kukamilisha kushughulikia sakata hilo lililogusa
mawaziri wa sasa na zamani, wanasheria wakuu wa Serikali, watumishi wa
umma na viongozi wa kidini.
Habari zaidi zinasema kuwa mkuu huyo wa nchi alikuwa na vikao tangu asubuhi.
Rais anatazamiwa kuondoka Jumapili kwenda nje ya nchi kwa safari za kikazi, kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari.
Shinikizo kubwa kwa sasa ni kumwondoa Waziri
Muhongo, ambaye Rais Kikwete alisema Desemba 22 mwaka jana kuwa
amemuweka kiporo kwa “siku mbili au tatu” kusubiri uchunguzi, lakini
mwezi mmoja sasa hakuna uamuzi uliofanywa dhidi ya mtaalamu huyo wa
miamba.
Tayari wabunge wa vyama vya upinzani wameshaeleza
kuwa watamwondoa kwa nguvu mbunge huyo wa kuteuliwa na Rais iwapo
atarejea bungeni Jumanne wakati Mkutano wa 18 wa Bunge utakapoanza mjini
Dodoma, wakati mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), Zitto Kabwe amesema Bunge halitampa ushirikiano waziri huyo na
kwamba atakuwa na kazi ngumu wakati wa Bunge la Bajeti katikati ya
mwaka.
Profesa Muhongo anatuhumiwa kutoshughulikia vizuri
sakata la escrow na kusababisha Serikali ikose fedha kwa njia ya kodi.
Juhudi zake za kujitetea bungeni ziliishia kwa wabunge kutoa vielelezo
kadhaa kuthibitisha hoja za kuhusika kwake kwenye sakata hilo.
Katika sakata hilo, zaidi ya Sh306 bilioni zilichotwa kwenye akaunti hiyo iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT). Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa pamoja na Shirika la Umeme
(Tanesco) na Kampuni ya IPTL, ambayo iliingia mkataba wa kuliuzia umeme
shirika hilo la umma, baada ya pande hizo mbili kuingia kwenye mgogoro
wa viwango vya tozo na hivyo kufungua kesi mahakamani.
Kesi hiyo iliisha kwa jaji kutaka pande hizo mbili
zikokotoe upya viwango vya tozo hiyo, lakini fedha zote zilizokuwamo
kwenye akaunti hiyo zikaondolewa mwishoni mwa mwaka juzi na kulipwa kwa
Kampuni ya Pan African Power
Solutions (PAP), ambayo ilinunua hisa zote za umiliki wa IPTL. Wakati
malipo hayo yanafanyika, kulikuwa na pingamizi la Mamlaka ya Mapato
(TRA) ambayo ilitaka kodi ambayo Tanesco ilitakiwa ilipe, ikatwe kwanza
kabla ya IPTL kulipwa fedha zake, huku ikihoji kodi nyingine katika
ununuzi wa hisa za kampuni nyingine iliyomiliki kwa muda hisa za IPTL ya
Piperlink ulioonekana kutawaliwa na udanganyifu.
Tayari Fredrick Werema, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, ameshajiuzulu wadhifa huo, wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya
Madini na Nishati, Eliackim Maswi amesimamishwa kazi kwa ajili ya
uchunguzi.
Pia, wabunge watatu waliokuwa wenyeviti wa kamati
za Bunge, William Ngeleja, Andrew Chenge na Victor Mwambalaswa,
wanaotakiwa kuachia nyadhifa zao, ikiwa ni sehemu ya maazimio ya Bunge.
Wabunge hao ni miongoni mwa mlolongo wa viongozi wa umma, vigogo wa
zamani wa Serikali na watumishi wa umma walioingiziwa fedha na mmiliki
wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James Rugemarila ambazo zinahusishwa na
kashfa hiyo au kutotangaza maslahi binafsi katika vikao vilivyohusu
sakata hilo.
Chenge, mbunge wa Bariadi ambaye alikuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, aliingiziwa Sh1.6 bilioni, Ngeleja Sh40.4
milioni, wakati Mwambalaswa ameondolewa kutokana na kuwa mwenyekiti wa
Kamati ya Nishati na Madini na wakati huohuo akiwa mwenyekiti wa Bodi ya
Tanesco iliyotuhumiwa kushindwa kushughulikia vizuri sakata hilo.
0 comments:
Post a Comment