pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Usafiri: Hivi ndivyo Malori yaua maelfu ya watu nchini



 

Dar es Salaam. Jitihada za Serikali na wadau wengine kupunguza ongezeko la ajali nchini, zimeendelea kupambana na vikwazo baada ya kubainika kuwa malori yanachangia sehemu kubwa ya ajali hizo.Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili sehemu mbalimbali nchini, umebaini kuwa malori mengi ambayo yanasafirisha mizigo ndani na nje ya nchi, yamekuwa yakiegeshwa barabarani bila hadhari yoyote kwa wasafiri wengine na hivyo kusababisha ajali ambazo zinaua maelfu ya watu.
Takwimu za Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2010 hadi Machi mwaka huu, malori yalisababisha ajali 23, 746 na kusababisha vifo 2,413 na majeruhi 7,958.
Takwimu za Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2010 hadi Machi mwaka huu, malori yalisababisha ajali 23, 746 na kusababisha vifo 2,413 na majeruhi 7,958. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mwaka 2010 pekee, zilitokea ajali za magari 24,665 na kuua watu 3,582, kati ya hizo 3,134 zilisababishwa na malori na kuua watu 493 na kuacha majeruhi 1,926.
Ripoti hiyo ya Polisi inaonyesha kuwa mwaka 2011 kulitokea ajali 33,943 na kuua watu 3,981 kati ya hizo zilizosababishwa na malori zilikuwa 3,219. Mwaka huu malori yalisababisha vifo vya watu 506 na kuacha majeruhi 1,792.
Taarifa ya polisi inaeleza kuwa zaidi ya asilimia 10 ya ajali zilizotokea mwaka 2012 zilizababishwa na malori. Katika mwaka huo jumla ya ajali 33,115 zilitokea na kuua watu 3,969 kati ya ajali hizo 3,559 zilihusisha malori ambazo ziliua watu 692 na kuacha majeruhi 1,877.
Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2013 kulitokea ajali 34,344 na kuua watu 4,002 kati ya hizo zilizosabishwa na malori 3,561 na kuua watu 608 na majeruhi 2,075. Kwa mujibu wa takwimu hizo kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, jumla ya ajali 4,893 zilitokea na kuua watu 854 kati ya ajali hizo zilizosababishwa na malori zikiwa ni 655 ambazo zimeua watu 114 na majeruhi 288.
Jinsi malori yanavyosababisha vifo barabarani
Baadhi ya ajali kubwa zilizotokea mwaka huu na kuua watu wengi ambazo zimesababishwa na malori, tatu zilitokea mkoani Pwani na Singida.
Ipo ajali iliyotokea Machi 30 katika Barabara ya Moshi hadi Chalinze katika eneo la Hedaru Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, ilihusisha malori mawili na gari dogo aina ya pick-up na kuua watu 12 papo hapo waliokuwa wakienda msibani.
Kabla hata watu hawajasahau kilichotokea Same, ajali nyingine ilitokea Kata ya Mkupuka wilayani ya Rufiji Mkoa wa Pwani na kuua watu 21. Ajali hiyo ilitokea baada ya lori kugongana uso kwa uso na gari aina ya Hiace iliyokuwa ikitokea Ikwiriri kwenda Kibiti.
Hiace hiyo ilitaka kulipita lori lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara, lakini aligongana uso kwa uso na lori lingine na watu saba kufariki dunia papohapo, huku wengine 14 walikufa baada ya kugongwa na basi lililokuwa likitokea Mtwara wakati wakihudumia majeruhi kando ya barabara.
Ajali nyingine ni ile iliyotokea Mei 6, katika Kijiji cha Utaho, Tarafa ya Ihanja mkoani Singida na kuua watu 19.basi la Kampuni ya Sumry kuwagonga wanakijiji waliokuwa wamekusanyika kando ya barabara kushuhudia ajali iliyotokea kati ya mwendesha baiskeli aliyegongwa na lori na kufariki dunia papo hapo.
Jijini Dar es Salaam
Uchunguzi uliofanywa na Gazeti hili mbali ya malori hayo kusababisha ajali katika barabara za mikoani pia hata katika maeneo ya majiji likiwamo Jiji la Dar es Salaam.
Kuanzia Februari hadi Machi mwaka, zaidi ya malori 70 yalikwama na mengine kuanguka katika Barabara ya Kilwa kutoka Mbagala Rangi Tatu kuelekea Kongowe.
Barabara nyingine ambazo kila siku huwezi kukosa kuona malori yameharibika katikati ya barabara na mara nyingi kusababisha ajali jijini Dar es Salaam ni Barabara ya Morogoro na Mandela.
Christopher Mwita mkazi wa Mbande wilayani Temeke anailalamikia hali hiyo kwa kusema, huwa haamini kama kuna watu wanalipwa mishahara kwa ajili ya kuhakikisha barabara zinapitika bila kikwazo muda wote.
Mwita alisema kuna wakati anatumia saa nzima eneo hilo bila sababu kutokana na malori hayo kupaki katika maeneo ambayo hayajatengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Gazeti hili pia lilifanya uchunguzi katika kipande cha barabara kutoka Mtoni Mtongani hadi Mbagala Misheni, eneo hili linaongoza kwa ajali za malori yakiwamo ya mafuta. Kwa mwezi katika eneo hili zaidi ya malori 50 hadi 65, hukwama barabarani kutokana na ubovu, huku baadhi yake zikipinduka, kugonga magari mengine kutokana na breki za magari hayo kuwa mbovu na eneo hilo kuwa na mteremko na kona kali.
Katika Barabara ya Mandela pekee kwa siku kunakuwa na malori kati ya 15-30, yakiwa yameweka vituo katika maeneo yasiyo rasmi kiasi cha kufanya eneo hilo lionekane kama karakana.
TATOA yaweka msimamo
Akizungumzia adha hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori (TATOA), Seif Ally, anasema katika kuhakikisha hakuna vitendo kama hivyo kwa madereva kutoka katika chama chao wameanzisha mpango uitwao ‘Databank’, kwa ajili ya kuwa na taarifa za madereva wao wote.
Anafafanua lengo la mpango huo kuwa ni kusimamia nyendo zote za madereva wao wanaokiuka taratibu na kuvunja sheria za nchi ikiwamo kupaki maeneo yasiyoruhusiwa na kusababisha ajali kwa uzembe.
“Kupitia Databank, tutafuatilia vitendo vya madereva wetu popote pale walipo, wametoka wapi, wanafanya nini wakiwa nje ya ofisi ikiwamo na kusimamisha malori ovyo kitu ambacho kimekuwa ni tatizo sugu, pia tutasimamia ubora wa vitendea kazi ikiwamo kuhakikisha malori yanayotumika kusafirisha mizigo yana ubora unaokidhi viwango vya barabara za ndani na nje ya nchi,” anasema Seif.
“Ajali nyingi zinasababishwa na malori, lakini kuna uwezekano mengine siyo ya wanachama wetu, ingawa hilo halitukatazi kuchukua hatua kwa yoyote kwa mtu atakayeonekana kukiuka maadili ya udereva, ikiwamo kumpeleka kwa mamlaka husika ikigundulika kuwa siyo mwanachama wetu, kwa kuwa anatupaka matope,” anasema.
Madereva wa malori
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Malori, Rocket Matogolo anakiri kuwapo na ajali nyingi zinazosababishwa na malori, lakini anasukumia lawama kwenye miundombinu ya barabara kuwa mibovu.
Anasema miundombinu imekuwa kikwazo hasa alama za barabara, ambazo zinawekwa na baada ya muda zinatolewa pengine wezi na hakuna anayefuatilia baada ya hapo kitu kinachowafanya madereva kutembea bila kuwa na mwongozo.
Anataja upungufu mwingine unaowakwaza madereva waadilifu kuwa ni Polisi wa Usalama Barabarani kuwasimamisha mahali popote na kufanya ukaguzi bila kufahamu kuwa magari hayo ni makubwa na barabara nyingi ni nyembamba hivyo wakisimama wanaleta usumbufu kwa watumiaji wengine.
Matogolo anaitaja sababu nyingine inayowafanya wapate ugumu katika ufanyaji kazi wao pengine na kusababisha ajali kuwa ni kukosa maeneo ya kupumzikia wawapo safarini, kama ambavyo nchi nyingine zinafanya.
“Ukiingia nchini Zambia kila baada ya kilometa 30, kuna eneo la kupumzikia kama una usingizi, unataka kupiga simu, kuvuta sigara, lakini hapa kwetu hakuna ukianza safari hapa hadi Mwanza au Kigoma utapumzika kwenye mzani au ukikamatwa na trafiki,” alilalamika Matogolo.
Anasema maegesho pia ni kero kubwa, kutokana na kutakiwa kulipa wanapokamatwa wamepaki vibaya kiasi cha Sh 165,000-200,000, bila kuwapo na eneo maalumu wanalotakiwa kupaki.
Wasomi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika Shule ya Biashara, Dk Ulingeta Mbamba anasema, kama kuna nia ya dhati ya kupunguza ajali za malori ni kuhakikisha reli zinafufuliwa, zinaboreshwa na kuwa ndiyo njia kuu ya usafirishaji.
Anasema ukiachilia mbali kuwa ni salama, lakini pia ina gharama nafuu, lakini itapunguza kuharibika kwa barabara mara kwa mara ambazo hufanywa na malori
“Ukiangalia reli zimejengwa tangu miaka ya 1860, lakini hadi sasa zinatumika, hivyo kama kutakuwa na nia ya makusudi ya kuzikarabati zikafanya kazi ya usafirishaji, tutapunguza ajali na tutakuwa na uhakika wa mizigo mingi kwenda na kufika kwa wakati kunakohusika, ”alisema Mbamba.
Waziri wa Ujenzi
Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Gerson Lwenge anasema, kusimamisha malori maeneo yasiyo rasmi ni kinyume cha taratibu na wanaofanya hivyo wanatakiwa kuchukuliwa hatua na Mamlaka husika ikiwamo Wakala wa Barabara (TANROADS) na Halmashauri kwa barabara zilizopo chini yake.
Anafafanua hata zile zinazopita katika barabara za mitaani zinafanya makosa kwa kuwa barabara hizo haziruhusiwi kubeba mzigo zaidi ya tani 10, huku akishangazwa kuachiwa gari hizo kupita huko bila ya kuchukuliwa hatua.
Kuhusu Jiji la Dar es Salaam, Lwenge anasema kwa sasa wananchi wavumilie taabu wanayoipata wanapotumia barabara ya Mandela kwa kuwa ndiyo pekee inayotumika kutolea magari ya mizigo bandarini.
 chanzo, mwananchi

0 comments:

Post a Comment