pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Libya katika hali ya kutisha

Libya katika hali ya kutisha
Ushahidi wa mambo yote unaonesha kuwa hali nchini Libya imefikia hatua ya kutisha. Misri imeanzisha vita dhidi ya nchi hiyo huku kundi la Daesh nalo likiendelea kufanya jinai zake nchini humo. Kutekwa nyara raia 35 wa Misri ni habari nyingine mbaya iliyoakisiwa kutokea Libya. Umoja wa Ulaya kwa upande wake umesema, umeingia wasiwasi kutokana na hali ya hatari iliyoshadidishwa na jinai za kundi la Daesh huko Libya, suala ambalo ni hatari pia kwa usalama wa nchi za Ulaya. Umoja huo umezungumzia wajibu wa kuchukuliwa hatua za pamoja za wanachama wake ili kupambana na mgogoro wa Libya. Hata Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, hatua za kijeshi ni miongoni mwa njia zinazoweza kutumiwa ili kutuliza hali ya mambo nchini Libya. Tab'an amesema kuwa, hatua hiyo haiwezi kuchukuliwa bila ya idhini ya Umoja wa Mataifa. Hata hivyo jambo moja halikanushiki, nalo ni kwamba, jambo lolote lile linaweza kutokea nchini Libya, kwani hali katika nchi hiyo imevurugika mno. Jeshi la Anga la Libya limetangaza kufunga anga ya nchi hiyo. Wanajeshi wa Misri wamepelekwa kwenye mpaka wa Libya wakiwa katika tahadhari kubwa. Si hayo tu, lakini pia ndege za kijeshi za Misri zimefanya mashambulizi katika maeneo ya kundi la Daesh kwenye mji wa bandari wa Derna nchini humo, huku jeshi la Libya nalo likifanya mashambulizi dhidi ya kundi hilo kwenye miji ya Benghazi na Sirte. Kwa upande wa miundombinu ya Libya pia, hali ni mbaya mno. Hata shirika la taifa la mafuta la nchi hiyo huenda likasimamisha kusafirisha nje mafuta. Ni wazi kuwa Libya hivi sasa imo kwenye hali mbaya mno; hali ambayo tunaweza kusema kuwa, imechochewa na baadhi ya nchi za Magharibi. Madola hayo ni yale ambayo yaliona manufaa yao yamo katika kuitelekeza Libya baada ya kupinduliwa utawala wa Kanali Muammar Gaddafi. Baada ya kufanya mashambulizi ya kikatili yaliyoangamiza takriban miundombinu yote, nchi hizo wanachama wa NATO ziliitelekeza Libya zikihakikisha kuwa silaha zimeenea mikononi mwa watu na makundi yenye uhasama ambapo kila kundi lilikuwa linapingania kuwa na nguvu zaidi kuliko kundi jingine. Baadhi ya duru za kisiasa zinaamini kuwa shirika la kijeshi la NATO limeitumbukiza kwa makusudi Libya katika hali hiyo mbaya. Duru hizo zinaamini kuwa, madola ya Magharibi yanaweza kirahisi sana kudhibiti hali ya mambo nchini Libya kama yatataka kufanya hivyo. Ni jambo lililo wazi kwamba uzembe wa makusudi unaofanywa na nchi za Magharibi wa kuiacha Libya izame kwenye mgogoro wa miaka mitatu sasa, si jambo linalofanyika vivi hivi. Hivi sasa moja ya tatizo kubwa la kiusalama la Libya ni Daesh, kundi la kigaidi ambalo limeingia hadi katika kitovu cha mji mkuu Tripoli. Kundi jingine ni la Fajr la wapinzani wa serikali halali ya Libya ambalo limeungana na Daesh ili kujiimarisha. Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, Ni vipi Libya itaweza kupambana na makundi yenye silaha likiwemo kundi la Daesh linalopata msaada wa kila namna kutoka Magharibi na kutoka katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati wakati nchi hiyo haina jeshi lenye nguvu? Itaweza vipi kupambana na makundi hayo wakati ina serikali mbili na mabunge mawili hasimu? Kesho Jumatano, tarehe 18 Februari, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaitisha kikao kuzungumzia mgogoro wa Libya. Amma swali jingine linalojitokeza hapa ni kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi zilikuwepo wapi miaka yote hii mitatu ya mgogoro wa Libya ambao sasa umeingia kwenye hali mbaya sana?

0 comments:

Post a Comment