Serikali imesema wananchi 3,092 wamelipwa jumla ya
Sh 6.9 bilioni fidia kwa ajili ya kupisha ujenzi wa bomba la gesi
kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, ambalo ujenzi wake unatarajiwa
kugharimu Sh9.3 bilioni.
Taarifa iliyopatikana kutoka kwenye kitabu cha
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa kwa mwaka 2013/14, iliyotolewa na Ofisi
ya Rais, Tume ya Mipango ilieleza kuwa fedha hizo ni za ndani, ambazo
zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa maandalizi kwa ajili
ya ujenzi wa bomba la gesi lenye urefu wa km 532 (Mtwara-Dar es Salaam
na kipenyo cha inchi 36 yameanza, ambapo jiwe la msingi liliwekwa tangu
Novemba mwaka 2012.
“Mabomba yameshaanza kusambazwa katika njia
litakakopita bomba hilo, aidha fidia ya ardhi kupisha ujenzi
imekamilika, ambapo wanakijiji wapatao 3,092 wamelipwa,fidia ni Sh6
857,746,020,” ilielezwa katika taarifa hiyo.
Utekelezaji wa mradi wa mtambo wa kufua umeme
Kinyerezi (MW 240), umekwama kutokana na kuchelewa kwa majadiliano baina
ya Serikali na benki ya kimataifa ya Japan. Imeelezwa kuwa mradi
huo ambao unagharimiwa kwa mkopo kutoka katika benki hiyo ya Japan ambao
watachangia asilimia 85 na Benki ya Maendeleo ya Afrika Kusini ambayo
inachangia kwa asilimia 15.
“Ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kugharimu Dola za
Kimarekani 432,137,936, haujaanza kutokana na kuchelewa kwa majadiliano
ya mkopo baina ya Serikali na Japan na kigezo cha kufanya uhakiki wa
mradi kilichowekwa na Benki ya Afrika,” ilielezwa katika taarifa hiyo.
Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara
hadi Dar es Salaam ulizua mgogoro wa aina yake mwaka jana kati ya
wananchi na Serikali, baada ya wananchi wa mkoa huo waliungana na kuweka
itikadi zao pembeni ili kuupinga.
chanzo mwananchi
0 comments:
Post a Comment