Jambo linalosemwa mara nyingi ni
marekebisho ya kumi ya Katiba ya Zanzibar ambayo yanadaiwa kwenda
kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Suala hilo limezusha mjadala mkubwa
Tanzania Bara ambako inaonekana wamechukizwa na Katiba ile kutamka
kwamba Zanzibar ni nchi inayounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni wazi kuwa siyo sahihi kulaumu Katiba
ya Zanzibar kuwa imekosea kutamka kuwa visiwa hivyo ni nchi, kati ya
nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kifungu kinacholalamikiwa ni sura ya
1(1) inayoeleza Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote
la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyozungukwa
na bahari yake kama ilivyokuwa kabla ya 1964.
Zanzibar ina serikali yake ambayo ni
wazi kuwa inahitaji kuwa na sheria, watu, ardhi na mipaka kwani bila ya
mambo hayo serikali hiyo inafanyaje kazi wakati hata mipaka ya eneo
lake haijulikani?
Nguvu ya SMZ
Mipaka ya nguvu za SMZ kikatiba haina lengo la kupokonya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jiulize, SMZ itawezaje kutekeleza sheria zake ikiwa eneo la mipaka yake haikuainishwa katika katiba?
Kwa mfano, kuna meli inapita katika
eneo la pwani ya Zanzibar baina ya Tanzania Bara na Zanzibar, lakini
ilivyo meli hiyo ipo eneo la Zanzibar, ikamwaga mafuta machafu na
kuchafua mazingira. Je, sheria ipi inatumika katika kuishtaki meli hiyo
wakati suala la usajili wa meli siyo la Muungano?
Mfano mwingine ni kuwa kuna mtu
amekamatwa na Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) akiwa
na jahazi eneo la pwani ya Zanzibar akisafirisha karafuu kwa magendo, ni
sheria ipi itatumika ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au ya
Zanzibar?
Jawabu ni sheria ya Zanzibar. Sasa, je sheria hiyo mipaka yake inaishia wapi kama katiba haikuweka eneo la utawala wa Zanzibar?
Kwa maana hiyo, mtuhumiwa atashinda kesi
kwa hoja nyepesi kuwa mipaka ya Zanzibar haifahamiki, kwa hivyo
hakufanya kosa kwa sababu alikuwa haelewi wapi mipaka hiyo inaanzia na
kuishia kwa kuwa haipo?
Suala la mafuta na gesi asilia
limeamualiwa kuwa liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano kwa
maana hiyo kila upande utasimamia kwa sheria zake, ikiwa hivyo ndivyo ni
lazima eneo la mipaka ya kila upande ifahamike maana hakuna mwekezaji
atakayekuja Zanzibar kufanya utafiti wa mafuta ikiwa eneo la mipaka yake
haikuwekwa wazi.
Kwa kuwa suala la uchumi siyo la
Muungano kwa maana ya kila upande una wizara yake inayoshughulikia
uchumi, mipango na sera zake za uchumi na bajeti yake ni lazima iwepo
mipaka ya eneo la Zanzibar kwani wawekezaji wa miradi mikubwa
hawataweza kuwekeza miradi yao katika hali ya kutofahamika mipaka ya
utawala wa Zanzibar.
Pia, baadhi ya watu wamekuwa wakijenga
hoja kwamba Katiba ya Zanzibar katika mabadiliko yake ya kumi yamempa
uwezo Rais wa Zanzibar kuigawa nchi katika mikoa na wilaya, kinyume na
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hii, pia ni hoja ambayo imeshapitwa na
wakati. Mantiki ya kuwekwa kifungu hicho katika Katiba ya mwaka 1977
ilitokana na ukweli kwamba wakati huo kulikuwa na mfumo wa chama dola
ambao makatibu wa CCM wa mkoa ndiyo hao hao waliokuwa wakuu wa mikoa kwa
kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa
mwenyekiti wa CCM.
Jamhuri ya Tanganyika na ile ya Watu wa
Zanzibar ziliungana mwaka 1964 na ilipofika 1965 kulipitishwa kwa Katiba
ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Chini ya katiba hiyo, Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ikawekwa chini ya utawala wa chama kimoja cha
siasa, ingawa vilikuwa viwili, Zanzibar kulikuwa na Afro Shiraz Party na
TANU kwa Tanzania Bara.
Kwa kuwa suala la vyama vya siasa
halikuwa katika orodha ya mambo ya Muungano, vyama viwili ndivyo
vilivyosalia hadi ilipofika mwaka 1977, ASP na TANU vilipounganishwa na
kuzaliwa CCM.
Nadharia ya chama kushika hatamu
iliendelea na katika mfumo huo mihimili yote ya serikali ilikuwa chini
ya chama kimoja na ndipo katika katiba ya mwaka 1977 makatibu wa CCM wa
mikoa ndio hao hao waliokuwa wakuu wa mikoa.
Kama watu wanadai kuna ukiukwaji
umefanywa na Katiba ya Zanzibar, jambo moja wanalotakiwa kuelewa ni kuwa
hakuna katiba ndogo wala kubwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Zanzibar siyo jimbo
Zanzibar siyo jimbo kama yalivyo majimbo
katika nchi ya Australia au India ambapo zinaonyesha majimbo na
hazitakiwi kukiuka katiba.
Mfano hai ni kuwa hadi kufikia mwaka
2010, wakuu wa mikoa waliendelea kuwa wajumbe wa BLW Zanzibar wakati
Tanzania Bara, wakuu wa mikoa hawakuwa tena wabunge.
Suala la pili ni kwamba Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania anapoteua wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na
makatibu tawala wa mikoa na wilaya anafanya hivyo kwa ile ya Tanzania
Bara na siyo Zanzibar.
Tatu, Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi ndiye anayeteua wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na
maofisa tawala wa mikoa na wilaya na sina hakika kama ipo siku kabla ya
kuwateua aliomba idhini au kushauriana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika uteuzi wa nafasi hizo.
Ieleweke wazi kuwa Zanzibar siyo jimbo
la nchi yeyote badala yake ni nchi, ina watu wake na sheria zake kwa
mujibu wa mkataba wa Muungano wa mwaka 1964 ambao umelinda Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Serikali yeyote ile lazima iwe na eneo
lake la utawala ambalo limeelezwa katika katiba ya hiyo nchi. Kiini cha
tatizo hili la sasa kuhusu Zanzibar na katiba yao ni ukiukwaji
uliofanywa makusudi wa mkataba wa Muungano wa mwaka 1964.
Tusikwepe ukweli, watu wa kulaumiwa
katika hali iliyopo sasa ni wale waliochangia au kusababisha kero za
Muungano na kwa sababu hiyo sioni kama tunaweza kuepuka kuwa na muundo
wa Muungano wa serikali tatu.
Chanzo - Mwananchi
0 comments:
Post a Comment