Mwanasheria
mkuu wa serikali nchini Tanzania Jaji Fredrick Werema amesema hakuna
sheria inayompa mamlaka Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania
kulivunja bunge maalum la katiba hivyo amewataka umoja wa katiba ya
wananchi UKAWA kurejea katika bunge hilo kwa lengo la kupata maridhiano
ya pamoja.
Jaji Werema amesema hayo jana jijini Dar es salaam wakati alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kufafanua masuala kadhaa
yanayohusiana na mwenendo mzima wa Bunge Maalum la Katiba na madai ya
umoja wa katiba ya wananchi UKAWA.
Akitumia muda mwingi kufafanua baadhi ya vifungu katika sheria ya
mabadiliko ya Katiba, Jaji Werema amesema siyo kweli kwamba Bunge hilo
halina mamlaka ya kubadilisha vifungu vya Rasimu, na kusema kuwa kama
ingekuwa hivyo, basi kusingekuwa na haja ya kuwepo kwa Bunge hilo.
Kwa kutumia kifungu cha 25 cha Sheria hiyo, Jaji Werema amesema kuwa
Bunge hilo limepewa kazi ya kupokea Rasimu, kuijadili, kuiboresha, na
kutoa Katiba inayopendekezwa.
Amesema baada ya hapo, litatunga na kupitisha masharti ya mpito na
masharti yatokanayo bila kuingiliwa na mtu, kabla ya ukomo wake.
Kuhusiana na madai ya kwamba Rais anaweza kulivunja Bunge hilo, Jaji
Werema amesema kuwa Rais hana mamlaka hayo kabla bunge hilo halijamaliza
kazi yake na kwamba hakuna mtu yeyote mwenye uwezo huo kwa mujibu wa
sheria.
“Hakuna Ugunduzi mzuri uliowahi kufanywa na mwanadamu kama
ugunduzi wa Sheria na utawala wa Sheria, hayo ni maandishi tu lakini
lazima kila mtu ayafuate” Alisema Werema na kuongeza kuwa..
“Ninamuambia Rais kuwa Rais huna mamlaka ya kusimamisha Bunge la Katiba kwa mujibu wa sheria”
Werema ameongeza kwamba kama lengo la kusitisha vikao vya bunge kwa
ajili ya maridhiano, hakuna haja ya kufanya hivyo ka kuwa pande mbili
zinazolumbana, kila upande unang’ang’ania maslahi yake, hali
inayopelekea kusiwe na dalili za usuluhishi.
Kutokana na hilo, amesema kuwa msuluhishi pekee atakuwa ni mwananchi
wakati wa kupiga kura ya maoni na kwamba hivi sasa mjadala wa sura ya
Kwanza na Sita umekwisha fungwa.
Werema pia amekiri kuwepo na baadhi ya watu ndani ya CCM wenye
mtazamo tofauti lakini hawajasusia Bunge, na kwa kuwa wanafuata misingi
ya demokrasia, wakishindwa hoja zao, hukubaliana na hoja zinazoungwa
mkono na wengi.
0 comments:
Post a Comment