BARAZA LA MITIHANI
LA TANZANIA
UFAFANUZI
KWA UMMA KUHUSU KUTOJUMUISHWA KWA ALAMA ZA MASOMO YA HIARI KATIKA MATOKEO YA
MTIHANI WA KIDATO CHA SITA 2014
Baadhi ya wadau wamekuwa wakitaka kujua
utaratibu uliotumika kukokotoa pointi za madaraja katika matokeo ya Mtihani wa
Kidato cha Sita (ACSEE) 2014. Hii imetokana na kuona kuwa kuna baadhi ya masomo
hayakujumuishwa katika kupata idadi ya pointi kwa watahiniwa wa Tanzania Bara
na wale wa Zanzibar.
Baraza la Mitihani la Tanzania linapenda
kuwajulisha wadau wote kuwa ukokotoaji wa pointi za madaraja kwa watahiniwa wa
Mtihani wa Kidato cha Sita huzingatia masomo ya Tahasusi (Subject Combinations)
aliyoyasoma mtahiniwa kama ilivyobainishwa katika Kanuni za Mitihani (The
Examinations Regulations) Toleo la mwaka 2013 kifungu cha 23(1) kinachosomeka:
“The Advanced Certificate of Secondary
Education shall be awarded in four Divisions to both schools and private
candidates who have conformed to entry requirements and have fulfilled the
conditions of the awards. Calculations of points shall be done based on Subject
Combinations approved by the Ministry of Education”,
Masomo ya Tahasusi (Subject Combinations)
yanayotumika kukokotoa alama za madaraja
yamebainishwa katika Waraka Namba 1
wa mwaka 2006 wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi na Waraka Kumb. Namba P33/8/53/Vol.I/44 wa mwaka 2012 wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali, Zanzibar.
Baadhi ya Tahasusi zinazotumika Zanzibar
zinatofautiana na zilizopo Tanzania Bara, ambapo kwa Zanzibar zipo baadhi ya
Tahasusi zenye kuhusisha masomo ya hiari. Masomo ya hiari ambayo husomwa na
baadhi ya watahiniwa ni pamoja na
General Studies (GS), Islamic Knowledge, Basic Applied Mathematics (BAM),
Divinity, Computer Studies na Arabic Language. Hata hivyo, Baraza la Mitihani
hufanya tathmini na kutunuku ufaulu kwa masomo yote ya hiari ya mtahiniwa
katika cheti chake ili kimsaidie katika udahili wa ngazi mbalimbali za mafunzo
kulingana na matakwa ya sifa za mafunzo husika.
Taarifa za kina kuhusu utaratibu wa kutunuku
matokeo ya Kidato cha Sita zipo katika kitabu cha Mwongozo wa Matumizi ya Viwango vya Ufaulu na Utaratibu wa Kutunuku
Matokeo ya Kidato cha Nne na cha Sita kilichotolewa mwaka 2014. Aidha, kitabu hicho kilikabidhiwa
kwa Wakuu wa Shule zote za sekondari Tanzania
Bara na Zanzibar. Pia kitabu hicho kinapatikana kwenye tovuti ya Baraza la
Mitihani la Tanzania (www.necta.go.tz).
Baraza la Mitihani la Tanzania linawaomba
wadau wasipotoshwe na taarifa ambazo zinasambazwa katika baadhi ya vyombo vya habari na
mitandao ya kijamii ambazo zina lengo la kupotosha Umma.
Imetolewa
na,
AFISA
HABARI NA UHUSIANO
0 comments:
Post a Comment