Dar es Salaam. Fundi ujenzi, Yusuph
Abdallah ambaye amelazwa katika Taasisi ya Mifupa (Moi), ameeleza jinsi
alivyonusurika kifo baada ya jengo la ghorofa 16 kuporomoka Ijumaa
iliyopita.
Yusuph aliliambia Mwananchi akiwa wodini kwamba
kilichomponya ni neema za Mungu kwani kabla jengo hilo kuporomoka yeye
alikuwa ghorofa ya 15 kwenye jengo hilo katika Mtaa wa Indira Gandhi
akiendelea na ujenzi.
Alieleza kuwa hakuwa anafahamu kinachoendelea,
bali aliona ghafla jengo linaaanza kuporomoka, na baada ya hapo
hakufahamu zaidi kilichotokea hadi alipojikuta yuko hospitalini.
“Kweli jengo lilipoanza kuporomoka sikutambua nini
kinachoendelea kwani nilipoteza fahamu na kujikuta nipo hapa
Muhimbili,” anasimulia Abdallah.
Alisema anahisi alipoanguka alifunikwa na kifusi kilichomponda na kuvunja miguu yote.
Fundi huyo ambaye amefungwa plasta gumu (P.O.P) miguu yote, alisema hakuweza kuona watu waliomwokoa.
Mwingine aokolewa na mkewe
Mkazi wa Ubungo, Ally Mlela ambaye ni fundi
madirisha anasimulia jinsi mke wake alivyomwokoa katika ajali hiyo baada
ya kumtaka asiende kufanya kazi siku hiyo.
Akisimulia jinsi ilivyokuwa Mlela anasema siku ya
tukio aliwasiliana na rafiki yake ambaye amepoteza maisha katika ajali
hiyo na kumtaka aende akaonane na mkandarasi wa jengo hilo, ili ampe
kazi ya kuweka madirisha.
“Majira ya asubuhi kati ya saa mbili na saa tatu
hivi nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu jina maarufu anajulikana
kama Tafu, ambapo alinitaka niende nikaonane na mkandarasi wa jengo hilo
ili anipe kazi ya kuweka madirisha,” anasema Mlela.
Anasema wakati akijiandaa kutoka mke wake
alimwambia siku hiyo apumzike asiende kufanya kazi naye akakubali,
lakini haikupita muda mrefu mke wake alimfuata na kumuuliza amesikia
taarifa kwamba kuna jengo limedondoka?
“Niliamua kwenda katika eneo la tukio na ndipo
alipogundua kwamba eneo hilo ndiyo alipotakiwa kwenda kufanya kazi.
Wakati juhudi za uokoaji zikiendelea nilijaribu tena kumpigia simu
rafiki yangu.Nikiwa bado kwenye eneo la tukio ghafla nikaona mguu
ukitolewa kwenye mchanga na nilitambua ulikuwa mguu wa rafiki yangu
baada ya kuona kiatu chake.”
JK awatembelea majeruhi
Rais Jakaya Kikwete jana aliwatembelea majeruhi wa ajali hiyo ambao wamelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuwapa pole.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa
Tiba wa Taasisi ya Mifupa (Moi), Dk Cuthbert Mcharo alisema walipokea
majeruhi sita na hadi jana walikuwa wamebakia wanne.
Miili zaidi yapatikana
Katika hatua nyingine kikosi cha uokoaji jana
kilipata miili ya watu saba iliyopatikana. Mmoja kati ya miili hiyo
baada ya kuuchunguza, ulikutwa na kitambulisho cha kupigia kura
kinachomtambulisha kwa jina la Salumu Mwaliko kutoka Kijiji cha
Kwadeboma, Handeni mkoani Tanga.
Hatua hiyo inafanya idadi ya watu waliopoteza maisha katika maafa hayo kufikia 31.
NHC kugharimia majeruhi, mazishi
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick
alisema amepokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu kwamba kuna majengo matatu ya ghorofa
ambayo yanatakiwa kubomolewa kutokana na kuchakaa. Mbali na hilo, Mkuu
wa Mkoa amesema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linatakiwa kulipa
gharama zote za watu walioathirika na ajali ya Ijumaa iliyopita.
Alisema NHC wanapaswa kuwahudumia majeruhi wote pamoja na kugharimia mazishi ya watu waliopoteza maisha.
chanzo mwananchi
0 comments:
Post a Comment