
WIKI
moja baada ya Operesheni Safisha Jiji, baadhi ya wakazi wameomba Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq kuingilia kati, kuzuia
uvunjifu wa sheria wa kubomolewa baadhi ya nyumba za watu wasiohusika.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti jana, wakazi hao
walisema kama opersheni hiyo ikiachwa ifanyike bila kufuata sheria, kuna
hatari ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, na matokeo yake yakawa
mfano wa ile ya Operesheni Tokomeza Ujangili.
Walisema wasiwasi huo unatokana na baadhi ya askari kujiingiza kwenye
vitendo vya uhalifu kwa kuagiza nyumba za watu zivunjwe huku wakiondoka
na baadhi ya mali kusikojulikana.
Walieleza hawana tatizo na operesheni hiyo, bali wameitaka Kamati ya
Ulinzi ikiwa chini ya Mkuu wa Mkoa kuzingatia lengo maalumu la
operesheni hiyo.
Mkazi wa Mtaa wa Livingston, aliyejitambulisha kwa jina moja la
Amina, alisema kipande cha mbele cha nyumba yake kimevunjwa bila sababu
za kueleweka, kwani yeye si mfanyabiashara.
“Namuomba Mkuu wa Mkoa awe makini kwa sababu kuna askari ambao
walikuwa wanaipinga operesheni hii, sasa isije ikawa wanaihujumu kwa
makusudi ili isimamishwe wapate kuendelea na ufisadi wao wa kujipatia
fedha chafu kutoka kwa wamachinga,” alisema Amina.
Alisema ushahidi wa watu kubomolewa nyumba zao kinyume cha sheria
upo, kwa kuhakikisha hilo ni vema mkuu wa mkoa akafanya ziara ya
kujionea mwenyewe matukio hayo.
James Christopher, mkazi wa mtaa huo, alisema nyumba yake iko kwenye
eneo rasmi na wala haijawekwa alama ya X, lakini imebomolewa na askari
hao.
freemedia
0 comments:
Post a Comment